Mercy wanjau katibu wa baraza la mawaziri humu nchini amesema kwamba Kenya inatambua ujumuishaji wa walemavu.
Akizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa kongamano la kabla ya kongamano la ulimwengu kuhusu ulemavu katika hoteli moja jijini Nairobi, Wanjau alisema kwamba ujumuishaji wa walemavu upo kwenye katiba ya Kenya.
Wanjau alisema pia kwamba walemavu wamejumuishwa kwenye ruwaza ya mwaka 2030 na awamu ya nne ya mpango wa kati ya muhula wa mwaka 2023 hadi 2027.
Kulingana naye serikali ya Kenya inafahamu kwamba kujumuisha walemavu ni mojawapo ya mahitaji ya kuafikia malengo endelevu chini ya ajenda ya mwaka 2030.
Serikali kulingana naye inajibidiisha kuhakikisha kwamba walemavu ambao ni asilimia 2.2 ya idadi jula ya wakenya kulingana na sensa ya mwaka 2019, wamewajibikiwa kikamilifu na wanahusishwa kwenye maswala yote ya maisha.
“Hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha fursa sawa, ujumuishaji, haki na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.” Alisema Wanjau kwenye hotuba yake.
Alisema eneo la Afrika la kusini mwa jangwa la Sahara changamoto ya walemavu kutengwa inazidishwa na masuala kama wengi wao kuwa sehemu za mashambani, ulemavu kuathiri wanawake wengi zaidi ya wanaume, walemavu kuwa na viwango vya chini vya elimu na fursa finyu za ajira.
Bi. Wanjau alihimiza wanaohudhuria kongamano hilo la ulemavu barani Afrika la kujiandaa kwa kongamano sawia la ulemavu wajibidiishe kujumuisha walemavu.
Kongamano la ulimwengu la ulemavu litaandaliwa jijini Berlin nchini Ujerumani Aprili 2 na 3, 2025.