Hafla ya kutuza washindi wa tuzo za Pulse za watu wenye ushawishi mkubwa katika nyanja mbali mbali mwaka 2023 iliandaliwa usiku wa Jumamosi Oktoba 7, 2023.
Catherine Kamau maarufu kama Kate Actress aliibuka mshindi katika kitengo cha mitindo bora ya mavazi. Kwenye hotuba yake ya kukubali tuzo, Kate alitaja wasanifu wa mitindo ya mavazi ambao alisema wana wajibu mkubwa katika ushindi wake.
Mama huyo wa watoto wawili na ambaye alitengana hivi maajuzi na mume wake Phil The Director alikuwa na ushauri kwa waigizaji na waandaji video mitandaoni. Alisema kwamba hawawezi kujipiga kifua kwa ufanisi wa awali bali uzuri wao unategemea kazi zao zijazo.
Mwanariadha Ferdinand Omanyala bingwa wa mbio za mita 100 barani Afrika naye aliibuka mshindi katika kitengo cha mshawishi mkuu katika michezo.
Wixx Mangutha ndiye mshindi katika kitengo cha mpiga picha bora, Joanna Kinuthia mshindi katika kitengo cha urembo na mitindo ya maisha, Daddie Marto katika kitengo cha teknolojia na Cray Kennar katika kitengo cha mchekeshaji bora.
Washindi wengine wa tuzo hizo ni pamoja na Holy Dave katika kitengo cha maandalizi ya chakula, kundi la Alfa House katika kitengo cha densi, Terrence Creative katika kitengo cha mtandao wa Facebook naye Abel Mutua katika kitengo cha jukwaa la YoyTube kati ya wengine.
Tuzo za Pulse za watu wenye ushawishi huandaliwa kila mwaka kwa mwaka wa tatu sasa kwa nia ya kutambua na kuangazia jukwaa kubwa la ushawishi na ambao wamejenga jamii thabiti kulingana na nyanja ya kila mmoja.