Home Habari Kuu Kanisa latakiwa kuunga mkono vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati

Kanisa latakiwa kuunga mkono vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati

Naibu rais alilinganisha janga la matumizi ya pombe haramu na mihadarati na wakati virusi vya HIV na ugonjwa wa ukimwi duniani, ulikuwa janga la kimataifa.

0

Kanisa hapa nchini limetakiwa kupiga jeki vita dhidi ya utengenezaji, uuzaji, usambazaji na unywaji wa pombe haramu.

Akizungumza na viongozi wa makanisa waliomtembelea nyumbani kwake mtaani Karen jijini Nairobi, kwa mwaliko wa mkewe naibu rais pasta Dorcas, kujadili jinsi ya kupatanisha kanisa nchini kenya, naibu rais Rigathi Gachagua,  alitumia fursa hiyo kuelezea ajenda ya serikali kupiga vita pombe haramu nchini, na matumizi ya mihadarati.

Alielezea umuhimu wa jukumu la kanisa katika jamii, na ushawishi wake kama sauti inayotambulika, inapotiliwa maanani idadi ya waumini ambao viongozi hao hutangamana nao makanisani na kwenye hafla nyingine mashinani.

“Lazima mzungumzie maswala haya (Pombe haramu na mihadarati) kila Jumapili, kwa sababu wale wanaotumia, hawafanyi hivyo wakiwa nyumbani. Huku tunapo walaumu maafisa wa polisi na machifu, watu wetu pia wanahitaji kupewa mwongozo na ushauri nasaha kutoka kwa kanisa,” alisema naibu huyo wa Rais.

Naibu rais alilinganisha janga la matumizi ya pombe haramu na mihadarati na wakati virusi vya HIV na ugonjwa wa ukimwi duniani, ulikuwa janga la kimataifa, akisema mjadala kuhusu ugonjwa huo ulikuzwa, na hivyo kulipatia janga hilo mtazamo ufaao, kando na kuhakikisha uhamasisho kwa jamii.

“Tunawasihi katika muda wa miezi sita ijayo, mtenge muda katika mahubiri yenu kuzungumzia utumizi wa dawa za kulevya, kama sehemu ya kuwafahamisha watu wetu. Tunahitaji kanisa kutusaidia katika kampein hii,” aliongeza Gachagua.

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na na kasisi mkuu Among  Arthur Kitonga,  Gerry Kibarabara, kasisi Dkt. Margaret Wangari, Dkt. Mophat Kilioba, kasisi Dkt. Pius Muiru, Mchungaji Dkt. Lucy Muiru, mchungaji Paul Wanjohi, na Dkt. Stanley Michuki miongoni mwa wengine.

Website | + posts