Home Burudani Kanayo adai kuwa na hadhi ya juu kuliko Edochie katika Nollywood

Kanayo adai kuwa na hadhi ya juu kuliko Edochie katika Nollywood

0
Kanayo O Kanayo na Pete Edochie

Mwigizaji wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood Kanayo O Kanayo amedai kwamba hadhi yake ni ya juu kuliko mwenzake Pete Edochie katika tasnia ya filamu nchini Nigeria.

Kanayo anasema ukubwa wake katika tasnia hiyo hauwezi kupuuzwa kwani alianza kuigiza kwenye filamu hizo miaka minne kabla ya ujio wa Edochie hata ingawa Edochie amemzidi umri.

Aliyasema hayo kwenye video ambayo imesambazwa mitandaoni.

Nguli huyo wa uigizaji alitaja wengine na mafanikio yao katika tasnia hiyo kama vile Kenneth Nnebue ambaye anasema aliandaa filamu ya kwanza ya kitaalamu nyumbani mwaka 1992.

Alisema atapinga kwa dhati iwapo mtu angeandika simulizi la Nollywood na kumtaja Pete Edochie kuwa mkubwa kwake katika tasnia ya uigizaji.

“Katika Nollywood mimi ni mkubwa wake. Hili sio suala la umri.” alisema Kanayo.

Kanayo O Kanayo ambaye jina lake halisi ni Anayo Modestus Onyekwere, anafahamika sana kwa kuigiza kama mtu anayeamini na kutumia sana matambiko.

Alianza kuigiza mwaka 1982 huku Pete Edochie akianza kuigiza mwaka 1985. Ana umri wa miaka 61 huku Pete akiwa na umri wa miaka 76.

Video ya Kanayo inaaminika kuchochewa na matamshi ya Pete Edochie ambaye alisema kwenye mahojiano kwamba katika uigizaji, yeye ni mkubwa hata kuliko tasnia nzima ya Nollywood.

Alisema kwamba akiigiza kitabu cha “Things Fall Apart” mwaka 1985, Nollywood haikuwa imeanzishwa.

Website | + posts