Home Kaunti Kampuni ya maji ya Nyeri yapoteza fedha nyingi kupitia wizi wa vifaa

Kampuni ya maji ya Nyeri yapoteza fedha nyingi kupitia wizi wa vifaa

Kampuni ya maji na usafi ya Nyeri inapoteza mamilioni ya fedha kutokana na wizi na uharibifu wa vifaa vyake mjini Nyeri na maeneo yaliyo karibu.

Kufuatia hasara kubwa iliyokumba kampuni hiyo katika muda wa miezi mitatu iliyopita, maafisa wa usalama wa kampuni hiyo pamoja na maafisa wa polisi wamekamata washukiwa kadhaa ambao wameshtakiwa mahakamani.

Katika mkutano na wanahabari mjini Nyeri, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya maji na usafi ya Nyeri Mhandisi Peter Kahuthu alisema maeneo ambayo yameathiriwa sana na uharibifu na wizi wa vifaa ni Skuta,Ruringu na King’ong’o.

Kahuthu alisema kando na kupoteza fedha maji yanamwagika sana na hivyo kuathiri uzuri na usafi wake.

Aliomba wakazi wa Nyeri wawe macho na waripoti visa vya uharibifu wa vifaa kwa maafisa wa polisi au wakamate washukiwa na kuwapeleka kwa maafisa wa polisi.

Hata ingawa wanashirikiana na maafisa wa polisi, Kahuthu alisema anaamini iwapo wananchi watashirikishwa tatizo hilo ambalo linawaathiri litakabiliwa kabisa.

Kahuthu alisema pia kwamba kando na vifaa vya kupitisha maji safi, wezi wamekuwa wakiharibu mashimo ya maji taka pia wakilenga vyuma vilivyoko huko ili wakauzie wanunuzi wa vyuma chakavu.