Home Habari Kuu Kampeni ya Afya Nyumbani yafikia kaunti ya Narok

Kampeni ya Afya Nyumbani yafikia kaunti ya Narok

0

Kampeni ya upatikanaji wa huduma za afya kwa jina #AfyaNyumbani imefikishwa katika kaunti ya Narok.

Katibu wa afya ya umma katika wizara ya afya Mary Muriuki alikuwa katika lokesheni ndogo ya Ngoben wadi ya Ololunga kaunti ya Narok ambako alisisitiza umuhimu wa mpango huo wa #AfyaMashinani, jukumu la wahudumu wa afya ya jamii katika kuhakikisha usalama wa jamii kiafya.

Katika mkutano na wananchi wa eneo hilo, katibu Mary Muriuki alijadiliana nao kuhusu mipango kadhaa ya afya ya jamii na utekelezaji wa mpango wa huduma za afya kwa wote.

Waligusia pia kuanzishwa kwa mitandao ya afya ya msingi na sheria nne mpya za afya na maana yazo kwa wananchi.

“Tulijadili pia kuhusu umuhimu wa chanjo katika kupunguza vifo vya watoto na tukakubaliana kuhusu njia za kupunguza hatari za kiafya hasa msimu huu wa mvua.” alisema Mary.

Kulingana naye, kuna haja ya usafi stahiki, matumizi ya vyoo, kutupa taka kwa njia mwafaka na mikakati mwafaka ya usafi.

Baada ya mkutano huo, katibu Mary Muriuki alijiunga na afisa mkuu wa maswala ya afya katika serikali ya kaunti ya Narok Jane Kiok ambaye alikuwa ameandaa hafla ya kutoa shukrani.