Home Habari Kuu Kamati ya majadiliano kuanza kupokea maoni ya wadau Ijumaa

Kamati ya majadiliano kuanza kupokea maoni ya wadau Ijumaa

0

Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano  itaanza kupokea maoni kutoka kwa washikadau mbalimbali kuanzia Ijumaa wiki hii.

Hii ilibainika baada ya wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na kinara wa walio wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Muyoka kukutana Bomas of Kenya leo Jumatatu.

“Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano imedhamiria kukuza majadiliano ya wazi na jumuishi yatakayoongoza mustakabali wa nchi yetu,” alisema Ichung’wah baada ya mkutano wa hii leo.

“Tunaamini kabisa katika nguvu ya kuhusika kwa umma, na katika dhamira yetu ya uwazi na ushirikiano, tutaanza kupokea maoni ya washikadau Ijumaa wiki hii.”

Suala la kujazwa kwa nafasi nne za makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC linatarajiwa kuibua mdahalo mkali katika majadiliano ya kamati hiyo.

Mchakato wa kujaza nafasi hizo ulianza mwezi Februari ukiendeshwa na jopo linaloongozwa na Dkt. Nelson Makhandia.

Dkt. Makhandia na sekretariati ya IEBC inatarajiwa kuwa miongoni mwa washikadau watakaofika mbele ya kamati inayoongozwa na Ichung’wah na Kalonzo.

Mchakato wa kuunda upya tume ya IEBC ulisimamishwa punde baada ya kubuniwa kwa kamati ya kitaifa ya maridhiano.

Masuala ya kupanda kwa gharama ya maisha na uangaziaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 yanatarajiwa pia kuwa chanzo cha mdahalo mkali kwenye tume hiyo.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amenukuliwa akisema suala la uangaziaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 halipaswi kujadiliwa na kamati hiyo.

Website | + posts