Home Habari Kuu Kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya maridhiano yawasilisha ripoti kwa viongozi

Kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya maridhiano yawasilisha ripoti kwa viongozi

0

Kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya maridhiano imekamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa njia ya kielektroniki kwa viongozi wa pande zote mbili.

Kulingana na taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari, wenyeviti wa kamati hiyo Kimani Ichungwa na Kalonzo Musyoka wameorodhesha mapendekezo ya kamati hiyo kwa kiongozi wa chama tawala Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Mapendekezo ya kamati hiyo yako chini ya nyanja tano ambazo ni haki ya kiuchaguzi, gharama ya maisha, kuratibishwa kwa hazina za kitaifa kikatiba, kubuniwa na kuratibishwa kikatiba kwa afisi mbali mbali na uaminifu kwa sheria ya vyama vingi nchini.

Kuhusu haki ya uchaguzi kamati hiyo inapendekeza kuchunguzwa kwa mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kurekebishwa kwa kamati ya uteuzi wa makamishna wa tume ya uchaguzi nchini IEBC kutoka wanachama 7 hadi wanachama 9, kuongezwa kwa muda wa kutatua kesi ya kupinga uchaguzi wa urais kutoka siku 14 hadi 21 na kuratibisha kwamba mabadiliko ya sheria za uchaguzi yanayofanywa ndani ya miezi 18 kabla uchaguzi mkuu yasiathiri uchaguzi wa wakati huo bali uchaguzi unaofuata.

Kuhusu gharama ya maisha, kamati ya maridhiano inataka serikali ipunguze kwa asilimia 50 matumizi yake hasa kwa marupurupu ya usafiri wa maafisa wa serikali na kwa asilimia 30 matumizi yao ya kila siku.

wizara za kawi na fedha zimetakiwa kukubaliana kuhusu namna ya kupunguza ushuru wa kukarabati barabara kutoka shilingi 5 hadi shilingi tatu kwa kila lita ya mafuta.

Serikali kuu nayo imetakiwa kuhamisha majukumu yote yaliyogatuliwa na katiba hadi kwa serikali za kaunti nalo bunge lirekebishe kiwango cha mgao wa hazina ya usawazishaji kwa kaunti kutoka asilimia 15 ya fedha zinazokusanywa na serikali kuu hadi asilimia 20.

Kamati hiyo hata hivyo ilikosa kuafikiana kuhusu masuala kadhaa ya gharama ya maisha kama vile kupunguzwa kwa ushuru ziada wa thamani kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8.

Kuhusu hazina ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge, kamati ya maridhiano inapendekeza hazina hiyo na ile ya maendeleo katika wadi ziratibishwe kisheria kupitia bunge.

wawakilishi hao wa pande mbili za siasa nchini walipendekeza kwamba afisi ya kiongozi wa upinzani ibuniwe kisheria na kiongozi huyo atakuwa kiongozi wa chama kikubwa au muungano mkubwa uliopata kura nyingi baada ya chama tawala.

Walikubaliana pia kwamba afisi ya waziri mkuu ibuniwe kisheria.

Kamati hiyo imependekeza kubuniwa kwa kamati huru ya kusimamia vyama vya kisiasa ambayo itahusika na usajili wa vyama vya kisiasa, wasimamizi wa vyama hivyo na usimamizi wa hazina ya vyama vya kisiasa.

Kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya maridhiano ilibuniwa kama njia ya kusuluhisha matatizo yaliyowafanya wakenya kufanya maandamano yaliyokuwa yaliongozwa na Raila Odinga na iliratibishwa kisheria ba bunge la taifa na bunge la seneti.

Website | + posts