Kamati ya bunge kuhusu ulinzi, ujasusi na mambo ya nje, imeimarisha uchunguzi wake dhidi ya madai ya kikosi cha wanajeshi wa Uingereza wanaofanya mazoezi hapa nchini (BATUK).
Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Nelson Koech, siku ya Jumanne ilimhoji Esther Njoki Muchiri, ambaye ni mpwa wa marehemu Agnes Wanjiru, anayedaiwa kufariki mikononi mwa wanajeshi wa Uingereza.
Katika kikao hicho, Muchiri alielezea ghadhabu yake kuhusu kucheleweshwa kwa kesi hiyo ambayo imejikokota, licha ya kuwasilisha malalamishi mwaka mmoja uliopita.
“Tulituma malalamishi kwa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai mwaka jana. Mbona hatupati matokeo?” alishangaa Njoki.
Kamati hiyo pia iliwahoji wawakilishi kutoka shirika moja lisilo la kiserikali la Africa Centre for Corrective and Preventive Action (ACCPA), linaloendesha shughuli zake katika kaunti za Samburu na Laikipia.
Shirika hilo lisilo la kiserikali lilinakili visa kadhaa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu vinavyodaiwa kutekelezwa na BATUK, ikiwa ni pamoja na kisa cha kifo cha mkazi Robert Seuri, kilichosababishwa na kilipuzi, na mtoto Lisoka Lessuyan, aliyejeruhiwa na kilipuzi.
Aidha kamati hiyo pia ilielezea wasiwasi wake kuhusu madhara ya kimazingira yaliyosababishwa na wanajeshi hao, ikiwa ni pamoja na vilipuzi vya ardhini na kemikali aina ya phosphorus katika maeneo ya chemichemi za maji.
Kelvin Kubai, ambaye ni mshauri wa kisheria wa shirika hilo lisilo la kiserkali, alielezea haja ya jamii ya eneo hilo kuhusishwa kufuatilia visa vya dhuluma za kimapenzi vinavyohusishwa na wanajeshi hao wa Uingereza.
“Tunataka kufidiwa, haki na uponyaji wa kijamii ili kurejesha uhusiano kati ya wanajeshi wa Uingereza na jamii ya eneo hilo,” alisema Kubai.
Kamati hiyo inatarajiwa kuwahoji maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wale wa kuhifadhi mazingira NEMA na maafisa wa huduma kwa wanyamapori KWS, katika juhudi za kusuluhisha maswla yaliyoibuliwa.