Shirika la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji Nchini, KALRO limeanzisha mpango wa kina ili kuongeza kupatikana kwa mbegu zilizoidhinishwa kote nchini.
Kupitia mpango uliopewa jina Mkulima Shop, shirika hilo la serikali linapanga kufungua maduka 16 kote nchini ili kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora zilizoidhinishwa.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazao katika shirika hilo Felister Makini alisema hatua hiyo inalenga kupunguza uhaba wa mbegu zilizoidhinishwa nchini.
Aidha, alidokeza kuwa wakulima watawezeshwa kupanda mbegu bora katika maeneo yao ili kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula.
Makini alisema shirika hilo limetayarisha mbegu bora na aina bora za mimea ambayo itapatikana kwa wakulima kote nchini kupitia mpango huo wa Mkulima Shop.
Mbegu hizo ni pamoja na zile za mahindi, mpunga, mbaazi, soya, pamba na mtama. Uhaba uliopo wa mbegu zilizoidhinishwa umesababisha wafanyabiashara walaghai kuwapunja wakulima kwa kuwauzia mbegu duni.