Home Habari Kuu Kalonzo Musyoka alaumu polisi kwa kurushia jaji mkuu wa zamani gesi ya...

Kalonzo Musyoka alaumu polisi kwa kurushia jaji mkuu wa zamani gesi ya kutoa machozi

0

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amewalaumu maafisa wa polisi kwa kumrushia jaji mkuu wa zamani Willy Mutunga gesi ya kutoza machozi.

Kisa hicho kilitokea Jumamosi Julai, 8, 2023, katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi, wakati Mutunga aliongoza wanaharakati wa haki za binadamu hadi kituoni humo kutafuta kuachiliwa kwa waliokamatwa kwa kushiriki maandamano ya siku ya Saba saba.

Kupitia kitandazi cha Twitter, Kalonzo alisema kwamba serikali imejishusha sana kwa kutekeleza kitendo kama hicho. Kalonzo ambaye ni mmoja wa viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, anahisi matendo ya polisi dhidi ya raia wakati wa maandamano ya Saba Saba ni jaribio la kuharibu yote yaliyoafikiwa miaka 13 baada ya kuzinduliwa kwa katina mpya na miaka 30 tangu kurejeshwa kwa siasa ya vyama vingi.

Jumamosi wanaharakati kadhaa waliandamana hadi kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi wakiwa na lengo moja, kuhakikisha wenzao wanaachiliwa huru. Waliingia kwenye kituo hicho cha polisi huku wakiimba nyimbo za kutafuta haki ambapo walifahamishwa kwamba wenzao wapatao 75 watafikishwa mahakamani Jumatatu.

Waliagizwa na maafisa wa polisi waondoke na walipokosa kutii maafisa hao wa polisi wakawarushia gesi ya kutoa machozi.

Waliokuwepo ni jaji mkuu wa zamani Willy Mutunga, wakili John Khaminwa, wakili Lempaa Soyinka, wawakilishi wa shirika la kutetea haki za binadamu na wengine wengi. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu linataka uchunguzi ufanyike kuhusu madai kwamba maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano ya saba Saba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here