Home Kimataifa Kalonzo ajitangaza kuwa kiongozi mpya wa upinzani

Kalonzo ajitangaza kuwa kiongozi mpya wa upinzani

0
kra

Kalonzo Musyoka mmoja wa viongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya amejitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani kufuatia uzinduzi wa uwaniaji wa Raila Odinga wa uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC leo.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari wakati uzinduzi wa azma ya Odinga ulikuwa unaendelea katika Ikulu, Kalonzo alisema kwamba muungano wa Azimio unasalia imara hata baada ya Odinga kuamua kushirikiana na Rais William Ruto.

kra

Hatua ya Odinga kulingana na Musyoka imesababisha viongozi wa muungano wa upinzani wakosolewe vikali.

Naibu huyo wa rais wa zamani alikuwa ameandamana na viongozi wa baadhi ya vyama tanzu vya muungano wa Azimio akisema kwamba hiyo ndiyo sura mpya ya upinzani nchini.

Alikiri kwamba hawana wanachama wengi bungeni lakini imani yake ni katika wakenya ambao ni wengi.

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa chama cha Wiper alimsifia Odinga akisema yeye ndiye anafaa kuchaguliwa kuongoza AUC kwa sababu ya kujitolea kwake kwa masuala mbali mbali ya bara Afrika.

Musyoka alisema ushirikiano wa Odinga na serikali ya Kenya Kwanza inayogharamia kampeni yake hautakomesha upinzani kutekeleza wajibu wake wa uangalizi wa serikali ya Rais Ruto.

Kalonzo alisisitiza kwamba muungano wa Azimio hautavunjiliwa mbali na kwamba kutokuwepo kwake ikulu ni ishara tosha kwamba amejitolea kuwa kiongozi rasmi wa upinzani nchini.

Website | + posts