Home Habari Kuu Kalonzo aikosoa Kenya Kwanza kufuatia gharama ya juu ya maisha

Kalonzo aikosoa Kenya Kwanza kufuatia gharama ya juu ya maisha

0

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameisuta serikali ya Kenya Kwanza kutokana na kile ambacho ametaja kuwa kodi kubwa wanayotozwa Wakenya. 

Aidha amelalamikia kupandwa kwa gharama ya maisha ambayo amesema imewasababishia dhiki Wakenya wengi.

Akizungumza kwenye soko la Gakoromone katika kaunti ya Meru wakati wa ziara yake iliyoingia siku ya pili leo Jumatatu, Kalonzo akiwa ameandamana na Gavana wa zamani wa kaunti hiyo Peter Munya, aliulaumu utawala wa sasa akisema uliwalaghai Wakenya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita kwa kudai ungejali maslahi ya mtu wa kawaida.

Kalonzo alikuwa mwenyekiti mwenza wa kamati ya kitaifa ya uwiano pamoja na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah.

Kamati hiyo, miongoni mwa mambo mengine, ilikusudia kuangazia suala la kupanda kwa gharama ya maisha.

Hata hivyo, wakati ripoti yake ilipotolewa, suala la gharama ya maisha halikuwa miongoni mwa masuala yaliyoangaziwa na kusababisha migawanyiko katika muungano wa Azimio.

Viongozi Martha Karua wa chama cha Narc K na Eugene Wamalwa wa DAP-K ni miongoni mwa viongozi wa muungano wa Azimio waliopuuzilia mbali ripoti hiyo.

Kwa upande wake, serikali ya Rais William Ruto imepuuzilia mbali shutuma za upinzani ikisema imeweka mikakati kabambe inayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na hivyo kuchangia kupunguza gharama ya juu inayowakumba Wakenya.

Inatoa mfano wa bei ya mbolea ya bei nafuu inayosema imesababisha kuongezeka kwa mavuno miongoni mwa wakulima, hatua ambayo itaihakikishia nchi hii usalama wa chakula.