Home Habari Kuu Kaka watano wakamatwa kwa kuilaghai serikali ya kaunti ya Kwale

Kaka watano wakamatwa kwa kuilaghai serikali ya kaunti ya Kwale

Kulingana na EACC, washukiwa hao walikamatwa kuhusiana na wizi wa zaidi ya shilingi milioni 48.9.

0

Makachero wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi humu nchini (EACC), wamewakamata maafisa watano wa serikali ya kaunti ya Kwale kuhusiana na ufisadi.

Waziri wa fedha wa kaunti ya Kwale Vincent Mbito pamoja na ndugu zake wanne wanaofanya kazi katika idara mbalimbali katika kaunti hiyo, walikamatwa na maafisa hao Jumanne asubuhi.

Kaka hao ni pamoja na Mongo Mbito Mongo afisa msimamizi wa mapato katika kaunti, Hassan Shilingi Mbito, dereva anayehusishwa na kampuni ya huduma za maji ya Kwale, Mwaiwe Mongo Mbito, afisa wa ununuzi katika kaunti ya Kwale pamoja na Chindoro Mongo Mbito, mwajiriwa katika wizara ya afya na ambaye awali alikuwa mwanagenzi katika kaunti ya Kwale.

Kulingana na EACC, washukiwa hao walikamatwa kuhusiana na wizi wa zaidi ya shilingi milioni 48.9.

Kupitia kwa taarifa, familia ya akina Mbito ndio wakurugenzi au wamiliki wa kampuni za Chilongola Holdings na kampuni ya uwekezaji ya Rome ambazo zimetumiwa katika sakata ya wizi wa fedha za serikali ya kaunti ya Kwale.

EACC imesema watano hao watakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na kandarasi 10 zilizotolewa kwa kampuni hizo mbili.

EACC imeongeza kuwa fedha hizo ziligawanywa miongoni mwa washukiwa hao.

EACC imesema zabuni ambazo zilipatikana kupitia ukiukwaji wa sheria za ununuzi kwa kutumia hati ghushi, zilikuwa za utoaji na usambazaji wa sodo, chakula na vifaa vya afisi na taasisi.

Website | + posts