Home Kaunti Kahawa yageuka chungu Meru

Kahawa yageuka chungu Meru

Zao la kahawa ambalo awali lilitegemewa na wakulima wa eneo la Meru kama kitega uchumi kuwawezesha kuelimisha watoto na hata kukidhi mahitaji yao, limegeuka kuwa chungu huku wakikumbwa na matatizo ya kifedha.

Naftaly Kiambi, mwenyekiti wa chama cha ushirika cha wakulima wa kahawa cha Kaguru katika kaunti ya Meru anaelezea kwamba wasiwasi wake umeongezeka kufuatia marekebisho katika sekta hiyo.

Wiki jana alipata pigo baada ya kampuni ambayo chama chao hutumia kusaga kahawa yao kumwagiza akachukue magunia 600 ya kahawa ambayo walikuwa wamewasilisha huko.

Haya yanafuatia hatua ya kampuni hiyo ya kusaga kunyimwa leseni ya kuhudumu.

Walihamisha zao hilo hadi kiwanda cha KPCU kilichoko Dandora ambapo walipata gharama ya ziada ya shilingi laki 7.

Sheria mpya zilizobuniwa za kusimamia sekta ya kahawa hazikubalii kampuni moja kutekeleza hatua zote za kusaga kahawa, kuitafutia soko na kuinunua.

Hiyo ndiyo sababu kampuni kadhaa zilinyimwa leseni baada ya muda wa leseni za awali kukamilika Juni 30, 2023.

Wakulima sasa wanahisi kwamba marekebisho katika sekta ya kahawa yaliharakishwa na yanaumiza mkulima ambaye anafaa kufaidika kutokana nayo.

Chama cha Kaguru kilipata hasara tena Jumapili iliyopita baada ya wezi kuvamia maghala yake na kuiba magunia zaidi ya 100 ya kahawa ya thamani ya shilingi milioni 3.

Wezi hao walitekeleza uovu huo kunako saa nane asubuhi wakapakia shehena hiyo kwenye lori na kuondoka katika mchakato uliochukua takriban masaa mawili.

Wakulima hao wameachwa wasijue cha kufanya kwa sababu hawajapokea malipo kutokana na mazao yao huku msimu wa sherehe ukiwadia na Januari ikiwakodolea macho wakati watahitajika kulipia watoto karo.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts