Home Habari Kuu Kafyu kuendelea kutekelezwa Turkana

Kafyu kuendelea kutekelezwa Turkana

0

Maagizo yaliyotolewa na serikali ya kutotoka nje usiku katika maeneo mbali mbali ya kaunti ya Turkana yataendelea kutekelezwa, haya ni kwa mujibu wa waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki.

Alikuwa akizungumza katika bunge la Seneti alikofika kujibu maswali ya maseneta kuhusu jukumu lake kama waziri wa usalama wa taifa.

Swali kuhusu kafyu hiyo liliulizwa na Seneta wa Turkana James Lomenen aliyetaka kufahamu iwapo serikali imefanya utathmini wa athari za kafyu hiyo na ni lini itaondolewa.

Lomenen alitaja maeneo kama Kainuk, Lokichar, Kekunyuk, Kakongu, Kaputir, Kalengorok na Nakabosan.

Katika jibu lake, waziri Kindiki alisema kwamba kwa sasa hawezi kutangaza tarehe ya kuondoa maagizo hayo bali atafanya hivyo watakaporidhika kama wizara na hali ya usalama katika maeneo hayo.

Aliongeza kwamba utathmini wa hali umekuwa ukitekelezwa na wataangazia kila eneo kivyake na maeneo ambapo usalama utakuwa umeimarika yataondolewa maagizo hayo.

Hata hivyo waziri alisema kwamba kijumla maeneo hayo bado yanakumbwa na tishio la ukosefu wa usalama, tofauti na matamshi yake ya mwezi Machi mwaka huu ambapo alisema hali imeimarika, mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa “Operation maliza uhalifu”.

Website | + posts