Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege nchini, KAA inasema mazungumzo yameanzishwa yanayokusudia kuepusha mgomo ulioitishwa na Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege nchini, KAWU.
Chama hicho kimetoa ilani ya siku saba kikisema wanachama wake wataandaa mgomo kuanzia Jumatatu wiki ijayo kulalamikia mpango wa kukodisha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.
“KAA ingependa kuutarifu umma na washikadau wote kwamba tulipata ilani ya siku saba ya mgomo kutoka kwa KAWU siku ya Jumatatu, Agosti 12, 2024,” imesema mamlaka hiyo katika taarifa.
“Mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara ya Uchukuzi na Barabara, Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii, usimamizi wa KAA na KAWU kufikia makubaliano yanayokubalika.”
Mamlaka hiyo ikiongeza kuwa imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha shughuli zinaendelea kama kawaida endapo wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini watagoma kuanzia Jumatatu wiki ijayo.
Wafanyakazi hao wametishia kugoma baada ya miito yao ya awali kwa serikali kusitisha ukodishaji wa uwanja wa JKIA kwa kampuni ya Adani kutoka India kuambulia patupu.
KAWU inadai kwamba serikali haikufuata taratibu zilizoko kwenye katiba katika kuafikia mapatano na kampuni ya Adani kuhusu usimamizi wa JKIA.
Chama hicho kinasema Wakenya hawakuhusishwa katika ukodishaji huo inavyohitajika kikatiba na wafanyakazi wa uwanja huo wa ndege pia hawakuhusishwa.
Katibu Mkuu wa KAWU Moses Ndiema Ndiema anasema iwapo uwanja wa JKIA utakodishwa, wafanyakazi wako katika hatari ya kupoteza ajira kwani kampuni ya Adani inapanga kupunguza idadi ya wafanyakazi.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka ndiye alitangaza mpango uliopendekezwa kati ya serikali ya Kenya na kampuni ya Adani wa kukodisha uwanja wa JKIA.
Katika mpango huo, Adani itasimamia JKIA kwa muda wa miaka 30 na baada ya hapo itakabidhiwa kiwango fulani cha hisa kwenye umiliki wa uwanja huo.