Home Habari Kuu Jumwa: Wanawake wajumuishwe katika michakato ya amani

Jumwa: Wanawake wajumuishwe katika michakato ya amani

Wanawake hawapaswi tu kuhudhuria michakato ya amani, lakini sauti zao pia zinapaswa kusikika, kuheshimiwa na kujumuishwa katika viwango vya utoaji maamuzi.

0
Ipo haja ya kuwajumuisha wanawake katika harati za kuleta amani na usalama.

Waziri wa jinsia, utamaduni, sanaa na turathi Aisha Jumwa, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia tamaduni ambazo zinahujumu ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani na usalama hapa nchini.

Jumwa alisema taifa hili linapaswa kuendelea kuimarisha uwezo wa wanawake katika kuzuia mizozo na utoaji suluhu, akiongeza kuwa wanawake hawapaswi tu kuhudhuria michakato hiyo lakini sauti zao pia zinapaswa kusikika, kuheshimiwa na kujumuishwa katika viwango vya utoaji maamuzi.

Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na katibu katika idara ya jinsia Ann Wang’ombe wakati wa maadhimisho ya 23 ya maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa nambari (UNSCR1325), kuhusu wanawake na usalama na amani katika eneo la Iten, waziri huyo alisema usalama wa wanawake unapaswa kuhakikishiwa katika juhudi zao muhimu.

“Ushiriki wa wanawake sio tu swala la usawa, unahusu kuhakikisha juhudi za kuleta amani na usalama zinaimarishwa na kudumishwa,” alisema Jumwa.

Jumwa alisema wizara yake itashirikiana na serikali ya kaunti ya Elgeyo Marakwet, kupiga jeki ushiriki wa wanawake katika utoaji wa maamuzi, kutoa mafunzo kwa wanawake katika maeneo yanayokumbwa na mizozo.

Aidha waziri huyo alisema taifa hili Jumwa alisema taifa hili linatekeleza maazimio ya UNSCR1325, akitaja wanawake wanaofanya kazi katika asasi za usalama, waoshiriki katika kuleta amani na wanaokabilana na dhuluma za kijinsia, huku akisema mengi yanahitaji kufanywa.

Kwa upande wake Gavana wa kaunti ya Elgeiyo Marakwet Wisley Rotich, alisema huku serikali yake inkitia bidii katika kukabiliana na ghasia za kijinsia, imebuni sera ambazo zinasubiri kuidhinishwa na bunge la kaunti hiyo, kwa lengo la kuwajumuisha wanawake katika michakato ya kuleta amani.