Home Habari Kuu EAC yazindua programu ya mtandaoni kutathmini vituo vya mpakani

EAC yazindua programu ya mtandaoni kutathmini vituo vya mpakani

0

Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC imezindua programu ya mtandaoni ambayo itasaidia kutathmini ufanisi wa vituo vya mpakani 22 kote katika eneo hilo.

Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia maswala ya forodha, biashara na fedha Annette Ssemuwumba, alizindua programu hiyo kwa niaba ya katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Dr. Peter Mathuki, kwenye kikao cha ufunguzi cha awamu ya 14 ya kongamano la wadau wa sekta ya kibinafsi katika Umoja wa Afrika jijini Nairobi.

Ssemuwemba alitangaza kwamba programu hiyo iko tayari kwa matumizi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mpango wa kukusanya data, kuhamasisha kuhusu matumizi na kuanzisha kikamilifu matumizi yake utaanza hivi karibuni.

Vituo hivyo vya mpakani ni muhimu katika vivukio mipakani na vinachangia ukuaji wa biashara kati ya nchi wanachma kwa kupunguza gharama ya kufanya biashara kupitia kupunguza muda na gharama ya kuvuka mpaka. Vinasaidia pia kupunguza wingi wa stakabadhi sawia zinazohusishwa na urasimu kwenye vituo vya pande mbili mipakani.

Ukosefu wa data ya kusaidia kuchagua hatua za kuchukua kuhusu vipengee muhimu kama ufanisi wa vituo vya mpakani , watendakazi na hali ya vifaa umekuwa ukilemaza kuchukuliwa kwa hatua za pamoja ili kuhakikisha ufanisi zaidi wa vituo hivyo.

Utathmini wa vituo hivyo vya mpakani utaangazia maswala kadhaa kama vile muda ambao unatumika kukamilisha mipango ya kiutawala, kupunguza gharama ya usafirishaji, kupunguza gharama ya kuhesabu na kuongeza ukusanyaji wa mapato na biashara.

Maafisa wa forodha katika eneo la Afrika Mashariki watatumia data itakayokusanywa kupitia programu hiyo kutathmini ufanisi wa vituo vya mpakani na kubuni mikakati ya kuviboresha.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here