Home Habari Kuu Julius Bitok: Wakenya 58,330 hawajachukua Pasipoti zao

Julius Bitok: Wakenya 58,330 hawajachukua Pasipoti zao

Kwenye taarifa, Bitok alisema kuwa takriban pasipoti 58,330 hazijachukuliwa katika afisi mbalimbali za uhamiaji kote nchini.

0

Katibu katika wizara ya uhamiaji Julius Bitok, ametoa wito kwa wakenya ambao tayari wamepokea arifa za kuwafahamisha kuwa pasipoti zao ziko tayari, kwenda kuzichukua haraka iwezekanavyo, ili kutoa nafasi katika mfumo wa kuhifadhi stakabadhi hizo.

Kwenye taarifa, Bitok alisema kuwa takriban pasipoti 58,330 hazijachukuliwa katika afisi mbalimbali za uhamiaji kote nchini.

Nairobi inaongoza kwa kuwa na takriban paspoti 24,613, ambazo hazijachukuliwa, ikifuatwa na kaunti ya Embu, ambapo paspoti zipatazo 9,584 hazijachukuliwa.

Katibu Bitok alisema kuwa, idara ya kutoa huduma za uhamiaji imeimarisha shughuli zake za kutayarisha na kuchapisha paspoti, ili kukabiliana na mrundiko wa maombi ya stakabadhi hizo muhimu za usafiri.

Aliongeza kuwa maombi hayo yanashughulikiwa kwa kuzingatia maombi yaliyotumwa mapema, hasa kwa kuzingatia uwepo wa vitabu maalum vya kuchapisha paspoti, na pia idadi ya kurasa zilizolipiwa na kila anayetuma maombi.

Mwezi uliopita, waziri wa usalama wa taifa Profesa Kithure Kindiki, alielezea wasiwasi kuhusiana na kucheleweshwa kwa utoaji wa stakabadhi hizo muhimu za usafiri.