Home Kimataifa Judith Suminwa Tuluka ateuliwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa DRC

Judith Suminwa Tuluka ateuliwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa DRC

Waziri mkuu anaongoza serikali ambayo pia inaundwa na mawaziri na manaibu waziri.

0
Judith Suminwa Tuluka, ameteuliwa kuwa waziri mkuu wa DRC.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Félix Tshisekedi amemteua waziri wa zamani kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo.

Judith Suminwa Tuluka, aliyekuwa Waziri wa Mipango anachukua nafasi ya Sama Lukonde aliyejiuzulu mwezi Februari mwaka huu.

“Ninajua kwamba kazi ni kubwa na changamoto ni kubwa, lakini kwa uungwaji mkono wa rais na ule wa kila mtu, tutafika,” Tuluka alisema katika mkutano na wanahabari jana Jumatatu baada ya uteuzi wake.

Uteuzi huo unafuatia utafutaji wa muda mrefu wa muungano wa wengi katika Bunge la Kitaifa – hatua muhimu kabla ya Waziri Mkuu kutajwa na serikali kuundwa.

Chama tawala cha Union for Democracy and Social Progress kilipata nafasi ya wengi kikivishinda vyama vingine 44. Tuluka anatarajiwa kutaja baraza jipya la mawaziri wiki zijazo.

Waziri Mkuu anaongoza serikali ambayo pia inaundwa na mawaziri na manaibu waziri.