JSC yakosoa wanaoilimbikizia idara ya mahakama tuhuma za ufisadi

Martin Mwanje & Celestine Mwango
2 Min Read
Hakimu Mkuu Mwandamizi ambaye pia ni mwanachama wa JSC, Evelyne Olwande

Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imekashifu watu wanaokosoa idara ya mahakama kuhusu madai ya ufisadi ikisema kuwa walalamishi wanapaswa kuwasilisha ushahidi kwa tume hiyo ili iweze kuchukua hatua mwafaka. 

Matamshi hayo yametolewa na Hakimu Mkuu Mwandamizi ambaye pia ni mwanachama wa tume hiyo Evelyne Olwande wakati akizungumza mjini Migori.

Bila kumtaja Rais William Ruto moja kwa moja, Olwande alisema wamesikia tu madai ya viongozi wa kisiasa lakini walalamishi hawajawasilisha ushahidi wowote.

Rais Ruto ameapa kuangamiza ufisadi anaosema umekithiri katika idara ya mahakama, na amewakosoa majaji kwa kula njama na watu fulani kuhujumu utekelezaji wa miradi ya serikali.

Olwande ambaye aliongoza timu kutoka JSC alisema tume hiyo imeweza kushughulikia malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya majaji na mahakimu baada ya kupata ushahidi dhahiri unaowahusisha na makosa mbalimbali.

Matamshi yake yaliungwa mkono na Gavana wa kaunti ya Migori Ochilo Ayacko aliyesikitikia taarifa za jumla zinazotolewa dhidi ya mahakama.

Ochilo alisema mashambulizi yanayoelekezewa idara ya mahakama hayafai, akiongeza kuwa watu walio na malalamishi maalum wanapaswa kufuata njia mwafaka.

Wakati huo huo, tume hiyo imekubali kushirikiana na kaunti ili kuwasilisha huduma za mahakama kwa Wakenya wote.

Wanachama wa tume hiyo walisema wanataka kuhakikisha kuwa angalau kuna mahakama katika kila kaunti ndogo nchini ili kuimarisha haki na huduma Kwa wote.

Gavana Ayacko aliahidi kuwa serikali yake itatoa ardhi ambayo itatumiwa na tume hiyo kuanzisha mahakama katika kaunti hiyo.

Aliyekuwa Gavana wa kaunti ya Bomet ambaye pia ni mwanachama wa tume hiyo ya utumishi wa mahakama Isaac Ruto pia alitoa wito kwa serikali kuitengea idara ya mahakama pesa zaidi.

Ruto alilalama kwamba mahakama nyingi ambazo ujenzi wake ulianza miaka mingi iliyopita bado hazijakamilika kwa sababu ya uhaba wa fedha.

Martin Mwanje & Celestine Mwango
+ posts
Share This Article