Home Habari Kuu Jowie ahukumiwa kifo

Jowie ahukumiwa kifo

0

Joseph Irungu maarufu kama “Jowie” amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mfanyabiashara Monica Kimani mnamo mwaka 2018.

Akizungumza wakati wa kutoa hukumu hiyo leo Jumatano Machi 13, 2024, jaji wa mahakama kuu Grace Nzioka alisema kwamba mauaji ya kinyama ya marehemu Kimani yalitekelezwa kwa kupenda.

Nzioka aliendelea kusema kwamba Jowie hakutenda kitendo hicho kama njia ya kujikinga na hakuchochewa kwa vyovyote na mhasiriwa kutekeleza unyama huo.

Jaji huyo alitaja mawasilisho ya upande wa mashtaka wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo ambapo waligusia madhara mabaya mno aliyosababishiwa mhasiriwa kwa kutumia silaha waliyotaja kuwa hatari.

Jambo lingine alilogusia ni kwamba mauaji hayo yalikuwa yamepangwa kwani hakuna kiwango cha uchochezi ambacho kingemsukuma Jowie kumuua Kimani.

Mwezi jana Jowie alipatikana na hatia ya mauaji ya Kimani ambaye aliuawa kinyama katika nyumba yake huko Lamuria Gardens, Nairobi usiku wa Septemba 19, 2018.

Mshtakiwa mwenzake Jackie Maribe hata hivyo aliondolewa lawama kwenye kesi hiyo kwa kile ambacho mahakama ilitaja kuwa ukosefu wa ushahidi wa kudhibitisha kwamba alihusika kwenye mauaji hayo.