Rais William Ruto leo amepokea ripoti kutoka kwa jopo alilobuni la kuchunguza mfumo wa kisheria unaosimamia mashirika ya kidini nchini.
Kiongozi wa nchi alibuni jopo hilo mwezi Mei mwaka 2023 kupitia arifa za gazeti rasmi la serikali toleo la tarehe 5 na la 11 Mei 2023.
Chini ya uenyekiti wa Mchungaji Mutava Musyimi jopo hilo limeibuka na ripoti kuhusu mianya ya kisheria ambayo imeruhusu au huenda ikaruhusu kuchipuza kwa mashirika ya kidini yenye misimamo mikali.
Katika utangulizi wa ripoti hiyo, jopo hilo linaelezea kwamba limeibuka na sehemu nne muhimu katika uchunguzi wao na sehemu ya kwanza ni uchunguzi na mapendekezo na sehemu ya pili ni sera.
Sehemu ya tatu inahusu mswada uliopendekezwa na ya nne ni mswada wa kanuni.
Jopo hilo limependekeza pia mfumo wa kisheria, kitaasisi na kiutawala katika kukabiliana na mchipuko wa mashirika ya kidini ya kutiliwa shaka.
Kando na hilo, linapendekeza pia uhamasisho wa umma kuhusu dini na masuala ya uraia na kuwe na namna ya kupiga ripoti kuhusu mashirika mabaya ya kidini huku walinda usalama wakifahamishwa jinsi ya kushughulikia ripoti hizo.
Suala jingine lililopendekezwa ni kuwekwa kwa viwango vitakavyozingatiwa katika kusajili mashirika ya kidini na stakabadhi zinazohitajika.
Ikumbukwe kwamba mauaji ya Shakahola ndiyo yalisababisha kubuniwa kwa jopo hili baada ya kubainika kwamba mchungaji mmoja alikuwa analazimisha wafuasi wake kufunga kula na kunywa hadi kufa na miili yao kuzikwa katika msitu wa Shakahola.