Home Habari Kuu Jopo la kutathmini mashirika ya kidini lazuru Meru

Jopo la kutathmini mashirika ya kidini lazuru Meru

0

Jopo lililobuniwa na Rais William Ruto kuhakiki sheria na sera za kudhibiti mashirika ya kidini nchini lilizuru kaunti ya Meru kwa nia ya kupokea maoni kutoka kwa Wakenya hasa wahusika wa mashirika hayo ya kidini.

Waliohudhuria kikao hicho walikuwa na maoni kadhaa kama vile kuundwa kwa afisi ya usajili wa mashirika ya kidini na hivyo jukumu hilo kuondolewa kwenye afisi ya msajili wa vyama.

Walitaka pia afisi hiyo itakapoundwa, iwe na matawi katika kaunti zote 47 nchini.

Askofu Mark Kariuki, alielezea kwamba Wakenya wameghadhibishwa na mambo ambayo yanatekelezwa na mashirika fulani ya kidini nchini na tumaini lao sasa ni katika jopo hilo ili kuhakikisha matukio ya Shakahola hayatokei tena.

Mwezi Mei mwaka huu, Rais Ruto aliunda jopo la watu 17 na kulipa jukumu la kuhakiki sera zinazoongoza kubuniwa na kuendeshwa kwa mashirika ya kidini yakiwemo makanisa nchini Kenya.

Hatua yake ilichochewa na tukio la Shakahola ambapo kiongozi wa dhehebu la Good News International Paul Mackenzie amedaiwa kuwachochea wafuasi wake kususia chakula na wengi wao kuaga dunia.

Tangu wakati huo, miili zaidi ya 400 imefukuliwa katika msitu wa Shakahola, kaunti ya Kilifi na Wakenya kadhaa kuokolewa kutoka msitu huo ambapo walikuwa wanajinyima chakula na kufanya maombi wakitarajia kumwona Yesu.

Kiongozi wa kanisa hilo bado anazuiliwa na maafisa wa polisi huku mipango ya kutafuta makaburi na kufukua miili ikiendelea msituni hapo.

Jopo hilo linatarajiwa kukamilisha kazi yake mwezi Septemba na kutoa ripoti kwa rais.

Ripoti yake Jeff Mwangi.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here