Home Habari Kuu Jopo la kumchunguza Jaji Mohammed Kullow laapishwa

Jopo la kumchunguza Jaji Mohammed Kullow laapishwa

Jaji Mkuu Martha Koome ambaye aliongoza uapishaji huo, alitoa wito kwa jopo hilo kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria.

0

Jopo ambalo lilitwikwa jukumu la kuchunguza mwenendo wa jaji Mohammed Kullow na rais Ruto limeapishwa leo Jumanne.

Jaji Mkuu Martha Koome ambaye aliongoza uapishaji huo, alitoa wito kwa jopo hilo kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria.

Jopo hilo lina wanachama 12 ambao waliteuliwa na Rais Ruto mnamo Machi 8, 2024, kupitia gazeti la serikali. Mwenyekiti wa jopo hilo ni jaji wa mahakama ya rufaa Patrick Omwenga Kiage.

Kati ya majukumu yaliyopewa ni kuamua iwapo madai yaliyoibuliwa yanajumuisha ukiukaji wa katiba. Pia linatakiwa kuandaa na kuwasilisha kwa haraka ripoti na mapendekezo yake.

Kullow ambaye ni jaji katika mahakama ya Mazingira na Ardhi anasemekana kuchelewesha na kukosa kutoa hukumu kwenye kesi kadhaa wakati akiwa mahama za Narok.

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) iliwasilisha maombi ya kumwondoa jaji Kullow kwa Ruto ikisema kwamba kulingana na matokeo yake, misingi ya kikatiba ya kuondolewa madarakani imeafikiwa.