Home Kimataifa Joho: Ndio nilianguka mtihani wa kidato cha nne lakini nimebadili hali

Joho: Ndio nilianguka mtihani wa kidato cha nne lakini nimebadili hali

0
kra

Ali Hassan Joho ambaye ameteuliwa na Rais william Ruto kuwa waziri wa madini na uchumi wa baharini, amethibitisha kwamba kweli alianguka mtihani wa kidato cha nne lakini amebadili hali kufikia sasa.

Akizungumza mbele ya kamati ya bunge kuhusu uteuzi wakati wa usaili, Joho alisema alisumbuka sana kupata elimu wakati wake kwani alilazimika kufanya kazi ili kujilipia karo.

kra

Wakati akianza kutoa wasifu wake, Joho alielezea kwamba mpangilio wake huenda ukawa tofauti na wa wateule wengine wa uwaziri kwani alimaliza elimu ya shule ya upili, akaanza kazi ya biashara kabla ya kurejelea elimu ya juu.

Joho alitumia muda wake kuelezea jinsi alisomea kozi ya kuboresha ufaafu wake kwa elimu ya juu yaani Bridging Course, akasomea stashahada, ana shahada mbili na anaendeleza masomo ya shahada ya uzamili.

Alisema kwamba aliyemmotisha sana katika safari yake ya elimu ya juu ni Profesa Ali Mazrui ambaye hata baada ya kukosa kutimiza alama za kujiunga na chuo kikuu alipambana hadi akawa mmoja wa wataalamu wa elimu wanaoheshimiwa sana.

Kulingana na Gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Mombasa, suala la kiwango cha elimu yake ya juu limekuwa donda sugu maishani mwake na maelezo yake ya leo anaamini yatakomesha uvumi.

Aliongeza kwamba ana imani kwamba hivi karibuni atakamilisha masomo ya shahada ya uzamifu.

Joho ndiye wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo leo, siku ya mwisho ya usaili wa waliopendekezwa kuwa mawaziri na wateule wengine wanne watasailiwa leo.

Website | + posts