Mwigizaji wa filamu nchini Nigeria Jerry Williams ameondolewa kwenye chama cha waigizaji nchini humo almaarufu Actors Guild Of Nigeria – AGN kutokana na hulka yake ya kutumia dawa za kulevya.
Kiongozi wa kitaifa wa chama cha AGN Ejezie Emeka-Rollas alifichua kwamba chama hicho kimekuwa kikimfuatilia Jerry ambaye amekuwa akitumia dawa za kulevya tangu Disemba, 2022.
Anasema uanachama wa Williams ungesimamishwa kitambo lakini waliamua kumpa muda wa kupitia matibabu ili ajikomboe lakini amekuwa akirejelea dawa hizo.
Emeka Rollas anaelezea kwamba Jerry sasa ni hatari kwake binafsi na kwa waigizaji wenzake ambao huenda akatagusana nao kazini.
Alifafanua kwamba uanachama wa Jerry Williams umesimamishwa hadi atakapothibitishwa kuacha kabisa kutumia dawa za kulevya.
Thibitisho hilo alisema lazima litoke kwa kituo kinachofahamika cha kurekebisha watumizi wa mihadarati.
Katiba ya chama cha AGN hairuhusu wanachama kutumia madawa ya kulevya kwani chama kinaheshimu sheria za nchi ya Nigeria.
Chama hicho huwa kinashirikiana na afisi ya serikali ya kutekeleza sheria dhidi ya mihadarati yaani National Drug Law Enforcement Agency NDLEA. Mwaka 2022, wawakilishi wa afisi hiyo ya kupambana na matumizi ya mohadarati walizuru sehemu kadhaa za kuandaa filamu kuchunguza iwapo waigizaji na wahusika wengine walikuwa wanatumia mihadarati.