Home Habari Kuu Jenerali Ogola azungumzia siku 100 tangu kuteuliwa

Jenerali Ogola azungumzia siku 100 tangu kuteuliwa

0

Mkuu wa majeshi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla ametimiza siku 100 afisini tangu kuteuliwa kwake na Rais William Ruto baada ya kustaafu kwa mtangulizi wake, Jenerali Robert Kibochi.

Akizungumza kwenye mahojiano na runinga ya KBC, Ogolla alisema anataka kuacha jeshi thabiti, linaloheshimika kote ulimwenguni na ambalo litatekeleza wajibu wake popote wakati wowote.

Ogolla alisema ufanisi wake utapimwa kwa namna ambavyo jeshi litatekeleza majukumu yake huku akifupisha maono yake kwa maneno, “one force, one mission”.

“Kuweza kuleta watu wote pamoja, kuelewa jukumu letu na kuangazia lengo letu moja la kulinda uhuru wa nchi ya Kenya,” alielezea Ogolla kuhusu maono yake jeshini.

Angependa kuwezesha zaidi jeshi la Kenya na kulifanya kuwa la kisasa kwani majeshi kote ulimwenguni hukabiliwa na vitisho vipya kwa usalama kila kuchao.

“Tukipata kwamba baadhi ya vifaa vyetu na mikakati ina mianya basi tunaifanya ya kisasa na kuziba mianya hiyo ili kuhakikisha tunaweza kulinda nchi kila wakati.”

Kuhusu ufisadi unaoripotiwa wakati wa kusajili makurutu wa jeshi, Ogolla alisema wameweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha usajili huo unakuwa wa haki. Alitoa onyo kali dhidi ya yeyote atakayejaribu kujiunga na jeshi kupitia mlango wa nyuma.

“Sitaki mwanajeshi aliyelipa hela kujiunga na jeshi. Atahudumu vipi? Atailinda nchi yake vipi iwapo alilipa kuingia kwenye jeshi?” aliuliza Ogolla.

Idadi ya wanajeshi wa kike alisema inazidi kuongezeka na kwa sasa ni asilimia 17.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Francis Omondi Ogolla alikuwa akihudumu kama naibu mkuu wa majeshi.

Alijiunga na jeshi Aprili 24, 1984.