Home Michezo Jebet na Sawe ndio mabingwa wa mbio za nyika mwaka 2024

Jebet na Sawe ndio mabingwa wa mbio za nyika mwaka 2024

0

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya Kilomita 10 Agnes Jebet Ngetich na bingwa wa dunia wa nusu marathoni Sebastien Sawe, ndio mabingwa wa kitaifa wa mbio za nyika mwaka 2024.

Jebet amewashinda masogora wenzake katika shindano la kilomita 10 katika mbio za kitaifa za nyika ambazo pia zilikuwa za kuchagua kikosi cha kenya kwa mashindano ya dunia zilizoandaliwa Jumamosi katika uwanja wa chuo cha mafunzo ya maafisa wa magereza mtaani Ruiru.

Mbio hizo zilizokuwa na ushindani mkali zilishuhudia bingwa wa dunia Beatrice Chebet,mshindi wa Sirikwa Classic Emmaculate Anyango na Lilian Kassait wakibadilishana nafasi mara kwa mara.

Jebet akiwakilisha eneo la central Rift aliwatoka wenzake na kukata utepe kwa dakika 31 sekunde 50.9,akifuatwa na Anyango wa Nairobi katika nafasi ya pili kwa muda wa dakika 31 sekunde 53.1.

Kassait wa kutoka Magereza alimaliza wa tatu kwa dakika 31 sekunde 56 nukta 3, mbele ya Chebet aliyechukua nafasi ya nne.

Margaret Chelimo na bingwa wa Afrika Cynthia Chepng’eno walichukua nafasi za 5 na 6 mtawalia na kukamilisha nafasi 6 za kufuzu kwa mashindano ya dunia mjini belgrade Serbia.

Katika mbio za wanaume Sawe alikuwa na ushindani mkali kabla ya kuibuka mshindi kwa dakika 28 sekunde 38.3, akifuatwa na Samuel Chebolei, aliyeziparakasa kwa dakika 28 sekunde 38.9, huku Gideon Rono akimaliza katika nafasi ya tatu kwa dakika 28 sekunde 41.9.

Samuel Kibathi alitawazwa bingwa wa kilomita 8 wanaume chini ya umri wa miaka 20 kwa muda wa dakika 22 sekunde 37.7, akifuatwa na Charles Rotich kwa dakika 22 sekunde 8.9 huku Mathew Kipruto akiambulia nafasi ya tatu

Shindano la kilomita 6 wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 lilishindwa na Sheila Chebet kwa dakika 19 sekunde 30.4, Deborah Chemutai akamaliza wa pili kwa dakika 19 sekunde 31.8, naye Nancy Cherop akamaliza wa tatu.

Kikosi kilichoteuliwa kitaripoti kambini wiki ijayo kujianda kwa mashindano ya mbio za nyika ulimwenguni tarehe 30 mwezi huu nchini Serbia, ambapo Kenya itakuwa ikitetea taji ya jumla waliyotwaa mwaka jana mjini Burthurst Australia.

Website | + posts