Home Kimataifa Jamii yapongezwa kwa kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi

Jamii yapongezwa kwa kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi

Waziri wa afya Susan Nakhumicha, alizipongeza jamii za hapa nchini kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

0

Huku taifa hili linapojizatiti kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, jamii zimepongezwa kwa kutekeleza wajibu muhimu katika kukabiliana na maambukizi hayo

Waziri wa afya Susan Nakhumicha, alizipongeza jamii za hapa nchini kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, tangu ugonjwa huo kuripotiwa mara ya kwanza hapa nchini miaka 30 iliyopita.

“Jamii zimetekeleza jukumu muhimu kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuepusha maambukizi, matibabu na kuwatunza walioambukizwa virusi hivyo. Tunapoangazia kukabiliana na changamoto za virusi vya Ukimwi, tukumbuke wajibu unaofanywa na jamii wa kuleta mabadiliko,” alisema Nakhumicha.

Waziri huyo alisema kuwahusisha wahamasishaji wa afya ya jamii, kutasaidia kupunguza gharama ya kukabiliana na virusi hivyo.

Kulingana na Waziri huyo, jukumu la wahamasishaji hao wa afya ya jamii katika kupambana na kuenea kwa virusi vya Ukimwi ni pamoja na kuwaelekeza wananchi kupimwa hali yao ya HIV, kuwapa ushauri nasaha, kuhakikisha wanatunzwa vyema na kuandamana nao katika vituo vya matibabu.

Waziri huyo aliyasema haya Ijumaa katika kaunti ya Meru, wakati taifa hili lilijiunga na ulimwengu kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani.

Kwa upande wake, Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, alisema atashirikiana na utawala wa Rais William Ruto, kwa kuunga mkono juhudi za wahamasishaji wa afya ya jamii.

Maudhui ya mwaka huu ya siku ya Ukimwi duniani ni “Tuzipe fursa jamii kuongoza”.

Siku ya Ukimwi duniani iliadhimimishwa mara ya kwanza mwaka 1988.

Hapa nchini Kenya takriban watu milioni 1.3 wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Website | + posts