Home Habari Kuu Jamaa aliyeua watu wanne wa familia moja Kisumu akamatwa

Jamaa aliyeua watu wanne wa familia moja Kisumu akamatwa

0

Jamaa ambaye alipagawa na kudaiwa kuua watu wanne wa familia moja huko Muhoroni, kaunti ya Kisumu Jumamosi, Februari 24 usiku amekamatwa. Alikamatwa jana Jumapili usiku katika shamba moja la miwa.

Kulingana na taarifa ya maafisa wa polisi, mshukiwa wa umri wa miaka 28 alipatikana akiwa mnyonge baada ya kubugia kemikali inayotumiwa kuosha mifugo.

Polisi walimkimbiza kwenye hospitali ya kaunti ndogo ya Muhoroni ambapo amelazwa chini ya uangalizi mkali.

Kamanda wa polisi huko Nyanza Patrick Tito alisema watasubiri apone kisha apitie uchunguzi na baadaye kuchukuliwa hatua stahiki kulingana na sheria.

Tito alishukuru wananchi waliopasha polisi habari zilizofanikisha kukamatwa kwa mshukiwa akisema hawajafahamu kilichosababisha atekeleze mauaji hayo.

Jamaa huyo alichukua panga akaua mkewe aliyekuwa mjamzito na baadaye akaua mwanawe wa kiume wa umri wa miaka 6 waliokuwa wamelala kitandani.

Wengine waliouawa ni mjomba na shangazi wa mshukiwa.

Mshukiwa alihadaa mjombake wa umri wa miaka 70 atoke nje ili asaidie kutatua mzozo uliokuwa umezuka na alipotoka nje akamkata kichwani kwa panga mara mbili akafariki.

Mama wa umri wa miaka 58, mke wa mzee aliyeuawa naye aliuawa.

Majirani wamemtaja mshukiwa kuwa mpenda amani asiyetumia vileo vya aina yoyote wasijue kilichomsukuma kutekeleza uovu huo.