Home Habari Kuu Jamaa aliyeshambulia afisa wa polisi Roysambu akamatwa

Jamaa aliyeshambulia afisa wa polisi Roysambu akamatwa

0

Maafisa wa polisi wamemkamata jamaa ambaye alionekana kwenye video iliyosambazwa mitandaoni akimpa afisa wa polisi kichapo katika barabara ya Mirema, Roysambu jijini Nairobi.

Jamaa huyo kwa jina Ian Njoroge anaonekana akiwa amejawa na hasira huku akimshambulia afisa wa polisi kwa makofi na mateke hadi akamuangusha kwenye mtaro.

Njoroge alikamatwa kwenye makazi yake katika eneo la Jacaranda, Kayole kaunti ya Nairobi Jumapili usiku kwenye operesheni iliyoongozwa na maafisa wa upelelezi wa jinai, DCI.

Baadaye, video hiyo ilichapishwa ambayo inamwonyesha Ian akiwa amefungwa pingu huku akihojiwa na maafisa wa polisi waliokuwa wamemkamata. Amejitetea akidai kwamba afisa huyo aliitisha kiasi kikubwa cha hongo kilichomfanya akakasirike na kuamua kumshambulia.

Ian anafichua kwamba babake mzazi ni mwalimu wa shule ya upili na mamake ni mfanyabiashara kwenye video hiyo ambapo pia anasema kwamba hajapokea mafunzo yoyote ya kivita na ilikuwa mara ya kwanza kushambulia afisa wa polisi.

Polisi hao ambao sura zao hazionekani kwenye video hiyo wanasikika wakimwelekeza Njoroge ajitukane.

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu tukio hilo ambapo wengi wanamhurumia wakisema kwamba atatumiwa na maafisa wa polisi kama onyo kwa yeyote anayepanga kushambulia afisa wa polisi.

Website | + posts