Home Kaunti Jamaa akamatwa baada ya kumuua mtoto na kuwajeruhi wengine Nyandarua

Jamaa akamatwa baada ya kumuua mtoto na kuwajeruhi wengine Nyandarua

Wimbi la simanzi limetanda katika kijiji cha Matura eneo la Magumu huko Kinangop, kaunti ya Nyandarua baada ya mtu kudaiwa kumuua kwa kumdunga kisu mtoto wa jirani na kuacha wengine wawili na majeraha.

Mtoto aliyeuawa ni wa umri wa miaka miwili na waliojeruhiwa ni wa miaka mitatu na 16. Mwili wa mtoto huyo ulipatikana katika msitu ulio karibu na nyumbani baada yake kutoweka kwa siku mbili.

Mshukiwa wa uovu huo alikamatwa katika kijiji cha Gathwariga na wakazi waliokuwa wamejawa na hasira na ambao walichoma nyumba yake.

Kulingana na wakazi, mchukiwa kwa jina Kimani wa Kihiu ana sifa ya uhalifu katika eneo hilo na amewahi kukiri kuua na kujeruhi watoto.

Iliripotiwa kwamba yeye huhadaa watoto hao kabla ya kuwatendea maovu kama kisa ambapo alimbaka msichana wa umri wa miaka 16.

Watoto hao watatu ni wa familia tofauti za eneo hilo na wawili waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika hospital ya Naivasha level four.

Mzee wa kijiji Chege Kahuni, anasema wamekuwa wakitafuta watoto hao na wakapata mwili wa huyo mdogo na wawili wakaptikana wakiwa na majeraha mabaya ya kisu.

Mshukiwa alipatikana akizurura kwenye soko ya eneo hilo na alipokabiliwa akakiri kutekeleza uovu huo.

Kamishna wa kaunti ya Nyandarua Jardesa Abdikadir alithibitisha kisa hicho akisema mshukiwa amekamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Njabini.

Mbunge wa kaunti ya Nyandarua Faith Gitau alizuru eneo hilo baada ya kisa hicho na kuwataka maafisa wa polisi kuchukua hatua dhidi ya mshukiwa.

Aliongeza kusema kwamba serikali ni lazima ichukue hatua dhidi ya wahalifu wa aina hiyo ambao wanafaa kuondolewa katika jamii ili kuzuia visa kama hivyo siku za usoni.

Website | + posts
Lydia Mwangi
+ posts