Home Kimataifa Jaji Mkuu Martha Koome: Dhamira yetu ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wote

Jaji Mkuu Martha Koome: Dhamira yetu ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wote

0
Jaji Mkuu Martha Koome (kulia) akiwa ameandamana na Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola wakati wa uzinduzi wa mahakama katika kaunti ya Samburu
Jaji Mkuu Martha Koome (kulia) akiwa ameandamana na Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola wakati wa uzinduzi wa mahakama katika kaunti ya Samburu

Jaji Mkuu Martha Koome amekariri dhamira ya idara ya mahakama kuhakikisha watu wote wanapata haki kwa urahisi kila pembe ya nchi. 

Na ili kudhihirisha azima ya idara anayoiongoza, Jaji Koome amezindua jengo jipya la mahakama ya Maralal katika kaunti ya Samburu.

Wakazi wengi wa kaunti ya Samburu na kaunti za kaskazini mwa nchi wametaabika kupata haki kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa mahakama na miundombinu muhimu inayohitajika.

Katika kaunti Samburu, Jaji Koome aidha alizindua idara ndogo ya usajili, mfumo wa uwasilishaji kesi kwa njia ya kidijitali na mifumo mbadala ya usuluhishaji wa migogoro.

Jaji Koome akitumia fursa hiyo kusifia uzinduzi wa jengo la mahakama kuu alilosema ni ishara ya maono ya pamoja walio nayo ya kutekeleza mabadiliko ya kijamii kupitia upatikanaji wa haki.

“Hatuzindui tu jengo lililotengezwa kwa matofali. Badala yake, tunazindua mnara wa matumaini, nembo ya haki, na ushuhuda wa dhamira yetu isiyoyumba ya kuleta mfumo wa haki karibu na watu wetu,” alisema Jaji Koome.

Uzinduzi wa idara ndogo ya usajili ya mahakama kuu unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa umbali wa takriban kilomita 100 wanazosafiri walalamishi ili kuwasilisha kesi zao mahakamani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana wa kaunti ya Samburu Jonathan Lelelit alilalama kuwa Samburu ni moja ya kaunti kubwa zaidi nchini ilhali ina mahakama moja tu katika mji wa Maralal.

“Tuko tayari kupeana ardhi na kujenga mahakama katika maeneo ya Wamba na Baragoi lakini natoa wito kwa Jaji Mkuu kuwatuma mahakimu katika maeneo haya ili hasa washughulikie masuala ya ardhi,” alisema Gavana Lelelit.

Website | + posts