Home Kimataifa Jaji Mkuu Koome atoa maelekezo ya kuharakisha malipo ya faini na dhamana

Jaji Mkuu Koome atoa maelekezo ya kuharakisha malipo ya faini na dhamana

0
Jaji Mkuu Martha Koome
Jaji Mkuu Martha Koome
kra

Jaji Mkuu Martha Koome ametangaza maelekezo mapya ambayo yanadhamiriwa kuharakisha ulipaji wa faini na dhamana.

Maelekezo haya yanaondoa wasiwasi wanayokuwa nayo watumizi wa mahakama na yanatumia teknolojia kulainisha mchakato mzima.

kra

Mojawapo ya mabadiliko yaliyotangazwa ni kwamba utayarishaji wa malipo hayo utafanywa katika mahakama wazi hatua ambayo itaimarisha uwazi.

Hatua hii inawiana na ile ya mahakama kuanza kutumia teknolojia katika usimamizi wa kesi ambayo inawezesha malipo ya faini na dhamana kufanywa kwa njia ya kielektoniki.

Risiti na stakabadhi nyingine za hesabu za malipo huandaliwa kielektroniki na kurahisisha mpango mzima.

Ili kuhakikisha maandalizi ya malipo ya faini na dhamana kwa wakati, maombi ni lazima yawasilishwe kufikia saa tatu asubuhi na iwapo haiwezekani, kamati za watumizi wa mahakama zitatoa maelekezo.

Kila mahakama inayopokea maombi itakuwa na wasaidizi wawili, mmoja wa kusaidia hakimu katika majukumu mbalimbali na wa pili wa kushughulikia malipo ya faini na dhamana.

Washtakiwa ambao hawataweza kufanya malipo katika mahakama wazi, watapatiwa stakabadhi ya hesabu ya malipo na kupatiwa muda mwafaka wa kukamilisha malipo ya faini au dhamana.

Watakaokosa kulipa faini au dhamana kufikia saa 10 jioni siku ambayo wametoa ombi, watapatiwa hati za kujitolea kulipa.

Juhudi zimefanywa pia kuhakikisha udhibiti stahiki wa kifedha ambapo kila kituo cha mahakama kitakuwa na mhasibu aliyejukumiwa kukusanya mapato ya kila siku.

Kurugenzi ya teknolojia ya mawasiliano katika idara ya mahakama imejitolea kuhakikisha ustawishaji wa mifumo hiyo ya kielektroniki katika muda wa siku 30 ili kuimarisha ufanisi na upatikanaji. ‎

Maelekezo ya Jaji Mkuu ni hatua muhimu katika kuafikia idara ya mahakama iliyolainika na inayoendeshwa kielektroniki.

Website | + posts