Jaji mkuu Martha Koome amependekeza matumizi bora ya sheria na mbinu mpya katika kukabiliana na uhalifu uliopangwa wa kimataifa unaozidi kuongezeka pamoja na mitiririko haramu ya kifedha.
Akihutubia mkutano wa wadau wa idara ya mahakama kutoka nchi zipatazo 21 za Afrika huko Mombasa, Koome alisema uhalifu wa kimataifa na mitiririko haramu ya fedha sio matatizo ya kisheria tu bali pia ni tishio kwa jamii, chumi na mifumo ya utawala na yanahatarisha maono ya Afrika yenye ufanisi, thabiti na yenye amani.
“Kutoka Cape Town hadi Cairo, Dakar hadi Mogadishu, sote tumeona jinsi uhalifu wa kimataifa unavyovuruga jamii. Ulanguzi wa binadamu, biashara ya mihadarati, biashara ya sialaha haramu, uhalifu wa mitandaoni, uwindaji haramu, kugushi na uhalifu unaozidi kuongezeka wa kifedha vimekuwa kikwazo kwa maazimio yetu ya maendeleo.” alisema Koome.
Jaji mkuu alisema kwamba kulingana na afisi ya umoja wa mataifa kuhusu mihadarati na uhalifu, uhalifu uliopangwa wa kimataifa unachangia asilimia 2.7 ya pato jumla la ulimwengu huku thamani yake ya kila mwaka ikikisiwa kuwa Dola Trilioni 1.6.
Koome alisikitikia wanaoathiriwa zaidi na uhalifu katika jamii wakiwemo watoto wanaolanguliwa na jamii zilizoathiriwa zaidi na matumizi ya dawa za kulevya.
Aliomba idara za mahakama zitekeleze jukumu tajika zaidi katika kuadhibu wahalifu na kuzuia uhalifu uliopangwa wa kimataifa na mitiririko haramu ya fedha.
Alikariri haja ya mabadiliko ya kila mara na mafunzo ya kila mara kwa wadau wa idara ya mahakama ili waweze kushughulikia uhalifu ambao unabadilika kila wakati.
Jaji mahakama ya upeo nchini Ethiopia Tewodros Kebede, naye alisisitiza umuhimu wa kukuza sheria za kiasili za kukabiliana na uhalifu uliopangwa wa kimataifa na mitiririko haramu ya fedha.
Anaamini ni bora kujifunza hasa kutoka kwa majirani ambao wanashiriki mambo mengi akisema kwamba kwa miaka mingi, Afrika imekuwa ikitumia sheria za nje pamoja na taasisi ambazo haziwezi kusuluhisha matatizo yake ya kila siku.
Mkurugenzi wa taasisi ya masuala ya mahakama nchini Kenya Daktari Smokin Wanjala ambaye alizungumza kwenye mkutano huo alisema kwamba nchi zinapoimarisha mifumo ya kibinafsi ni muhimu kwa nchi hizo kushirikiana kutatua suala hilo.
Wadau wa taasisi za mafunzo ya masuala ya sheria na mahakama, majaji na watendakazi wengine wa idara hizo wa nchi mbali mbali za Afrika wanakongamana mjini Mombasa kwa siku tatu kujadili kuhusu changamoto na suluhisho mwafaka kwa tatizo la uhalifu uliopangwa wa kimataifa na mitiririko haramu ya fedha.