Home Habari Kuu Jaji Mkuu Koome: SRC, Mdhibiti wa Bajeti ni mwiba kwa utekelezaji haki

Jaji Mkuu Koome: SRC, Mdhibiti wa Bajeti ni mwiba kwa utekelezaji haki

0
Jaji Mkuu Martha Koome
Jaji Mkuu Martha Koome

Tume ya Mishaharra na Marurupu (SRC) na Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ni baadhi ya taasisi zinazodumaza utekelezaji wa haki nchini. 

Jaji Mkuu Martha Koome anailaumu SRC inayoongozwa na Lyn Mengich kwa kuingilia mamlaka ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kinyume cha katiba.

“SRC imeingilia mamlaka ya JSC chini ya kifungu 172(1)(b) cha katiba ambayo ni ‘kupitia upya na kutoa mapendekezo ya masharti ya utendakazi ’ ya wafanyakazi wa idara ya mahakama, ambayo yako nje ya mishahara na mafao ya maafisa wa serikali,” alilalama Jaji Koome katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na naibu wake Philomena Mwilu wakati wa mkutano wa kila mwaka wa majaji wa mwaka 2023 uliofanyika katika hoteli moja jijini Mombasa leo Jumatano.

Aidha anamnyoshea Mdhibiti wa Bajeti kidole cha lawama kwa kuweka vizingiti vinavyozuia utekelezaji wa Hazina ya Idara ya Mahakama.

“Hazina ya Idara ya Mahakama haifanyi kazi kikamilifu kama ilivyoelezwa kwenye katiba kwa sababu ya vikwazo vya urasimu na vizuizi vilivyowekwa na Mdhibiti wa Bajeti.”

Jaji Koome ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Juu sasa anasema idara ya mahakama inafanya mazungumzo na taasisi husika ili kutatua hali hiyo ya kutoelewana kwa mujibu wa katiba.

Ndani ya mahakama, Koome anasema uongezaji wa imani ya umma katika idara ya mahakama inasalia kuwa changamoto.

Anawataka majaji kuwajibika katika utendakazi wao ili kurejesha imani hiyo kupitia utoaji wa hukumu kwa wakati na kuwakabidhi wahusika hukumu hizo kwa wakati.

Mkutano wa kila Mwaka wa Majaji huratibiwa na kuandaliwa na Shule ya Idara ya Mahakama Nchini, (KJA).
Unawaleta pamoja majaji kutoka mahakama zote nchini na miongoni mwa mambo mengine kutoa kwao jukwaa la kufanya mazungumzo na kuakisi masuala ibuka yanayoiathiri idara ya mahakama.
Website | + posts