Rais wa Marekani Joe Biden amesema mashambulizi ya Israel huko Rafah “hayapaswi kuendelea bila mpango wa kuaminika wa kuhakikisha usalama” wa zaidi ya Wapalestina milioni moja waliokimbilia huko.
Amesema watu wengi waliokimbia makazi yao katika mji wa kusini mwa Gaza “wamefichuliwa na kuwa hatarini” na wanahitaji kulindwa.
Daktari wa Kipalestina mjini Rafah aliambia BBC watu waliokuwa hapo walikuwa wakiishi kwa hofu.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk anasema shambulio lolote litakuwa “la kutisha” na raia wengi “huenda wakauawa”.
Wiki iliyopita,Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa ameamuru wanajeshi kujiandaa kupanua operesheni yake ya ardhini hadi Rafah.Aliapa kuwashinda wapiganaji wa Hamas waliojificha katika mji huo.
Rafah imekumbwa na mashambulizi makubwa ya anga ya Israel katika siku za hivi karibuni, huku kukiwa na ripoti ya vifo.
Zaidi ya nusu ya wakazi milioni 2.3 wa Ukanda wa Gaza sasa wamesongamana katika mji huo kwenye mpaka na Misri, ambao ulikuwa na watu 250,000 pekee kabla ya vita kati ya Israel na Hamas kuanza mwezi Oktoba.
Wengi wa watu waliokimbia makazi yao wanaishi katika makazi ya muda au mahema katika mazingira duni, na upatikanaji mdogo wa maji safi ya kunywa au chakula.