Raia watano wa Marekani ambao walikuwa wamefungwa kwa miaka kadhaa nchini Iran, waliachiliwa huru kufuatia makubaliano ya mabadilishano ya wafungua yaliyoibua utata na ambayo yali simamiwa na Qatar.
Mabadilishano hayo yalifanyika baada ya dola bilioni sita za Marekani, ambazo awali zilikuwa mali ya Iran, zilizoshikiliwa nchini Korea Kusini, kuhamishiwa kwenye akaunti za nchi hiyo nchini Qatar, huku Iran pia ikitaka wafungwa wake walio nchini Marekani waachiliwe huru.
Raia hao wa Marekani wanaojumuisha mfanyabiashara na mwanamazingira waliondoka Iran wakiwa katika ndege ya Qatar na kusindikizwa na ndugu wawili na balozi wa Qatar.
Baada yao kuabiri ndege kuelekea nchini Qatar, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema;
“Leo hii, uhuru wao, uhuru wa raia hawa wa Marekani, waliofungwa kwa muda mrefu sana na kuwekwa kizuizini nchini Iran bila haki, una maana kwamba waume na wake, baba na watoto, babu na bibi, wanaweza kukumbatiana tena, wanaweza kuona kila mmoja. Wanaweza kuwa na kila mmoja tena.”
Mpango huo wa ubadilishanaji wa wafungwa uliafikiwa kwa upatanishi wa Qatar.
Katika tukio ambalo lilitazamwa kwa makini kote duniani, Iran ilitaka kuachiliwa kwa fedha zake takribani dola bilioni sita za kimarekani na kisha fedha hizo kuhamishiwa katika benki za Tehran nchini Qatar, huku ndege ya kuwabeba wafungwa hao ikiwa tayari muda wote mjini Tehran.