Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amejitolea kupatanisha Urusi na Ukraine akisema kwamba majadiliano na diplomasia ndizo njia pekee za kumaliza mzozo uliopo.
Modi alielezea kujitolea huko alipozuru Ukraine katika kile kinachochukuliwa kuwa ziara ya kihistoria.
Mwezi uliopita, Modi alizuru Urusi ambapo picha zilimwonyesha akimpiga pambaja Rais Vladimir Putin katika hatua iliyokashifiwa vikali na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.
Modi, mwenye umri wa miaka 73, anasema alipozuru Urusi, alimwambia Putin kwamba matatizo hayawezi kutatuliwa katika vita na kwamba ni lazima wahusika waketi pamoja na kutafuta suluhisho.
Alifika jiji kuu la Ukraine Kyiv kwa kutumia treni kutoka Poland, na Ijumaa ikawa zamu ya Zelensky kupigwa pambaja naye.
Sehemu ya kwanza ambayo Modi alipelekwa nchini Ukraine ni jumba la makumbusho la kihistoria ambapo alitizama maonyesho kuhusu watoto 570 wa Ukraine ambao wamefariki kwenye uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulioanza Februari, 2022.
Modi na Zelenzkyy waliweka vitu vya watoto kuchezea katika eneo hilo la makumbusho, huku Modi akisema moyo wake unasononeshwa na idadi ya watoto wasio na hatia waliouawa kwenye vita hivyo.
Wakiwa katika eneo hilo, Modi alimwekea Zelenskyy mkono kwenye bega, picha ambayo ilisambazwa mitandaoni.
Modi alisema India ilichagua upande wa amani katika mzozo wa Ukraine na Urusi na ndiposa amejitolea kuwa mpatanishi.
Hata hivyo, India haijawahi kuikemea Urusi kwa kuivamia Ukraine hatua inayochukuliwa kama ya kuunga mkono Urusi hasa ikitizamiwa kwamba India sasa imekuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Urusi wakati inakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi.
India ilihudhuria mkutano wa amani ulioongozwa na Ukraine nchini Uswizi mwezi Juni ambapo Zelenskyy alimtaka Modi akubali taarifa ya pamoja iliyounga mkono kuheshimiwa kwa mipaka ya Ukraine na nchi nyingine.