Home Kimataifa IGAD yapitisha mfumo wa sera za masuala ya vijana

IGAD yapitisha mfumo wa sera za masuala ya vijana

0

Mamlaka ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya serikali mbali mbali IGAD imepitisha mfumo wa sera kuhusu vijana katika mkutano wa mawaziri wa masuala ya vijana.

Mkutano huo wa mawaziri wa masuala ya vijana katika nchi wanachama wa shirika la IGAD uliandaliwa jijini Nairobi Septemba 27 2023, baada ya mkutano wa siku mbili wa wataalamu wa masuala ya vijana.

Mfumo huo wa sera kuhusu vijana wa shirika la IGAD ni nguzo muhimu katika kuimarisha haki za vijana katika eneo zima la IGAD na uliafikiwa baada ya mashauriano ya kina na wataalamu wanaohusika na masuala ya vijana katika nchi wanachama.

Sera hizo zinadhamiriwa kuongoza na kutoa kipaumbele kwa vijana katika sera, sheria na mipango inayolenga kuwapa vijana uwezo na kuhakikisha wanahusishwa kikamilifu katika mipango yote ya kisiasa.

Mkutano wa leo ulichochewa na ukweli kwamba eneo la IGAD linashuhudia ukuaji wa kiwango kikubwa wa idadi ya vijana ikilinganishwa na sehemu nyingine ulimwenguni.

Ndiposa ni muhimu kushughulikia changamoto za kipekee zinazowakumba vijana.

Wahusika wa mkutano wa leo ni pamoja na mawaziri wa masuala ya vijana kutoka mataifa ya Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.

Wataalamu wa masuala ya vijana katika mataifa hayo pia walihusika wakiwemo wawakilishi wa makundi ya kutetea vijana.

Website | + posts