Home Habari Kuu IEBC yatuzwa kwa kusimamia vema uchaguzi wa mwaka 2022

IEBC yatuzwa kwa kusimamia vema uchaguzi wa mwaka 2022

0

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC ndio mshindi wa Tuzo ya Usimamizi wa Uchaguzi 2023. 

IEBC pia ilituzwa baada kuibuka ya pili katika Tuzo ya Uchaguzi ya Ergonomic wakati wa halfa ya 19 ya Tuzo za Uchaguzi za Kimataifa iliyoandaliwa na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Ureno Novemba 15, 2023.

Hafla hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano na Kituo cha Kimataifa cha Masomo ya Bunge, ICPS.

“Hafla ya Tuzo ya Kimataifa ya Uchaguzi inasimama kama mnara, ikimulika jitihada za dhati na mafanikio ya kupigiwa mfano ya watu na mashirika katika nyanja ya uchaguzi. Hafla hii sio tu utambuzi wa mafanikio yao, ni sherehe ya azimio la pamoja la jumuiya ya uchaguzi,” alisema Matt Gokhool, Afisa Mttendaji wa ICPS.

Akipokea tuzo hizo, Afisa Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan aliishukuru ICPS kwa kuitambua tume hiyo.

“Pia nawatambua wafanyakazi wa IEBC kwa uadilifu wao, ushirikiano wao, kujitolea na utendakazi wao bora wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Bila shaka, mafanikio ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 yalitokana na juhudi za pamoja za kila mmoja wenu,” alisema Marjan.

“Hebu tujizatiti kuwa tume ya uchaguzi inayoaminika inayokidhi misingi ya demokrasia ya watu wa Kenya.”

Tuzo ya Usimamizi wa Uchaguzi hutambua hatua zilizochukuliwa na taasisi za usimamizi wa uchaguzi au maafisa wa usimamizi wa uchaguzi, mashirika ya kijamii na yale yasiyokuwa ya serikali na washikadau wengine kuzishinda changamoto mahsusi katika nchi mbalimbali, kusimamia vyema uchaguzi na kuhakikisha uchaguzi wa wazi unaoendeshwa kwa njia nzuri.

Tuzo ya Uchaguzi ya Ergonomic kwa upande mwingine hutambua hatua zilizochukuliwa na taasisi za usimamizi wa uchaguzi au maafisa wa usimamiaji wa uchaguzi, mashirika ya kijamii na yale yasiyokuwa ya serikali na washikadau wengine kwa kusudi la kuongoza michakato ya uchaguzi inayoangazia saikolojia ya wapiga kura na sifa mahususi za wapiga kura hao.

Wanaoteuliwa kuwania tuzo hizo hutoka nchi mbalimbali duniani.

Website | + posts