Home Habari Kuu Idadi ya waliofariki kufuatia mafuriko yafikia 136

Idadi ya waliofariki kufuatia mafuriko yafikia 136

0

Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El Nino zinazoshuhudiwa nchini kwa sasa imefikia 136. 

Hii ni baada ya watu 16 kufariki katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wizara ya Usalama wa Taifa inasema idadi ya familia zilizopoteza makazi ni 92,432.

“Kwa bahati mbaya, katika kipindi cha saa 24 zilizopita, vifo 16 vimeripotiwa na kuongeza idadi ya waliofariki hadi 136,” inasema wizara katika taarifa.

Huku athari za mafuriko zikiwa dhahiri, serikali inasema imepeleka boti katika kaunti za Mombasa na Garissa kusaidia katika juhudi za uokozi.

Wakati huohuo, serikali imeimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mafuriko katika kaunti ambazo zimeathiriwa mno na hali hiyo.

Leo Alhamisi, tani 10 za bidhaa mbalimbali za chakula zilisafirishwa kwa ndege hadi kaunti ya Wajiri wakati Vikosi vya Ulinzi Nchini, KDF vikipeleka chakula katika eneo la Chebaso, kaunti ya Isiolo.

Serikali inasema jumla ya kaunti 38 zimeathiriwa mno na mafuriko nchini.

 

 

Website | + posts