Home Habari Kuu Idadi ya waliofariki katika ajali ya mashua Senegal yafika 26

Idadi ya waliofariki katika ajali ya mashua Senegal yafika 26

Pwani ya Senegal ni miongoni mwa vituo ambavyo hutumiwa na maelfu ya wahamiaji kuelekea bara ulaya.

0
kra

Jeshi la wanamaji nchini Senegal, leo Jumanne limesema idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ya mashua siku ya Jumapili, imefika 26.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili baada ya mashua iliyokuwa imewabeba wahamiaji kuzama katika pwani ya nchi hiyo.

kra

Kupitia mtandao wa X, jeshi hilo lilisema lilipata miili 17 siku ya Jumanne, na kufikisha idadi jumla ya miili iliyopatikana kuwa 26, baada ya miili tisa kupatikana awali kufuatia ajali hiyo iliyotokea katika mji wa Magharibi wa Mbour.

Hata hivyo, jeshi hilo lilisema shughuli za kutafuta miili zaidi inaendelea, huku abiria wengi waliokuwa katika mashua hiyo wakiwa hawajulikani walipo.

Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, walisema watu wengi waliabiri mashua hiyo, ambayo ilipinduka muda mfupi baada ya kung’oa nanga.

Pwani ya Senegal ni miongoni mwa vituo ambavyo hutumiwa na maelfu ya wahamiaji kuelekea bara ulaya.

Mwaka huu pekee, zaidi ya wahamiaji 22,000 wamewasili katika visiwa vya Canary nchini uhispania, idadi ambayo ni maradufu ikilinganishwa na ile ya mwaka jana.

Website | + posts