Idadi ya Wakenya inakadiriwa kufikia milioni 70 katika muda wa miaka mitano ijayo, kulingana na Baraza la Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo, NCPD.
Kutokana na hilo, wapangaji na watunga sera wameombwa wakumbuke masuala ya ukuaji wa miji, uzazi na umri ili kujumuisha idadi ya watu katika mipango na utoaji huduma.
Naibu Mkurugenzi wa NCPD anayesimamia masuala ya elimu kwa umma na utetezi Jane Wanjaria amesema kwamba mitindo inayoibuka inaashiria kwamba Ruiru ni kati ya maeneo yanayoshuhudia ukuaji wa kiwango cha juu cha miji nchini.
Wanjaria amesema kwamba ni lazima wanaopanga mambo na kutunga sera wawaze kuhusu uzazi, ongezeko la haraka la idadi ya watu na idadi ya vifo na wapange ipasavyo mambo kama upatikanaji wa hospitali, maji na mahitaji mengine muhimu.
Naibu Mkurugenzi alikuwa akizungumza wakati wa utoaji wa stakabadhi kuhusu sera ya kitaifa ya idadi ya watu huko Juja kaunti ya Kiambu, hafla iliyohudhuriwa na manaibu kamishna wa kaunti na maafisa wa NCPD kati ya wengine.
Aliongeza kuwa data inaonyesha kwamba wanaume wana umri wa chini wa kuishi ikilinganishwa na wanawake. Wanaume wanaweza kuishi hadi umri wa miaka 61 na wanawake umri wa miaka 67.
Hali hii inaaminika kutokana na hatari nyingi ambazo wanaume hukumbana nazo hasa kazini.