Home Habari Kuu Ichung’wah aikosoa mahakama, aitaka isitumiwe kuhujumu mipango ya serikali

Ichung’wah aikosoa mahakama, aitaka isitumiwe kuhujumu mipango ya serikali

0

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah ameitaka idara ya mahakama kutokubali kutumiwa na wale aliowaita wahujumu uchumi kutatiza utekelezaji wa mipango ya serikali. 

Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu amesema kesi za sasa zilizowasilishwa dhidi ya mipango inayonuia kuinua kiwango cha maisha cha walala hoi na kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote nchini zinaonekana kukidhi maslahi ya wale wanaofaidika na hali ilivyo kwa sasa.

“Kesi hizi zinawasilishwa na matapeli wanaolenga kuzuia maendeleo badala ya kuhakikisha utekelezaji wa kweli wa haki,” alisema Ichung’wah wakati akizungumza huko Nyandarua.

Kesi kadhaa zimewasilishwa mahakamani kupinga utekelezaji wa mipango ya serikali ikiwa ni pamoja na mpango wa nyumba za gharama nafuu na fedha wanazotozwa watumishi wa umma kugharimia ujenzi wa nyumba hizo.

Kesi pia imewasilishwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Jamii, SHIF.

Rais William Ruto pia amelalamikia kile alichokitaja kuwa hatua ya watu fulani kutumia vibaya mahakama kuhujumu mipango ya serikali.

“Itabidi sasa tuwe na mjadala na watu ambao wanapeleka makesi kortini kuzuia maendeleo katika taifa letu la Kenya,” alisema Ruto.

Alilalamika kuwa watu hao wameteka maafisa fulani wa mahakama ili kulemaza juhudi za serikali za kuzuia wizi wa rasilimali za umma.

Kulingana naye, haina maana kwa watu wachache kuafikia matakwa yao huku umma ukiteseka.

Kiongozi wa nchi ameitaka idara ya mahakama ijitolee kufuata katiba na kuhudumia Wakenya.

Website | + posts