Hospitali ya rufaa na mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu imepandishwa hadhi na kuwa shirika la serikali.
Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo Daktari Richard Lesiyampe amesema kwamba mabadiliko hayo yatasaidia kuboresha utoaji huduma kwa watu.
Kulingana naye, taasisi hiyo ya afya inaendelea kutekeleza mpango wa kimkakati na ajenda ya mageuzi katika usimamizi ili kuboresha huduma za kiusimamizi na za matibabu.
Sasa anaitaka bima ya afya NHIF iongeze pesa inazolipia kila mgonjwa anayelazwa kutoka shilingi 3,500 hadi elfu 4,500 kwa kila siku akiongeza kwamba sasa kiwango cha hospitali hiyo ni 6A na inatoa huduma na utunzi spesheli.
Lesiyampe alitangaza kwamba leseni ya hospitali hiyo ya Jaramogi kutoka kwa bodi ya wahudumu wa afya na madaktari wa meno – KMPDB imetolewa upya ili kuimarisha hadhi yake kama taasisi inayoongoza katika utoaji huduma za afya na mafunzo.
Katika taarifa yake, Lesiyampe alifafanua pia kuhusu mipango ya kuongeza idadi ya vitanda hadi 760 ili kuhakikisha inakidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka ya huduma za afya.
Hatua ya kupandisha hadhi taasisi hiyo ya afya ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Gavana wa kaunti ya Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o awali.
Katika tangazo la gazeti rasmi la serikali kuhusu kupandishwa hadhi kwa hospitali hiyo, umuhimu wake kama hospitali ya zamani zaidi na iliyoendelea sana katika eneo hilo umetajwa.
Inahudumia watu wapatao milioni 10.