Timu ya wavulana ya kaunti ya Homa Bay na ile ya wasichana ya kaunti ya Busia ndizo zimeshinda mashindano ya soka baina ya kaunti ya Talanta Hela kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 19.
Wavulana hao wa Homa Bay walishinda wenzao wa Kisumu kwenye fainali na wasichana wa Busia wakashinda wale wa Kisumu mabao matatu kwa moja kwenye fainali zilizochezwa leo katika uwanja wa taifa wa Nyayo.
Rais William Ruto ameshiriki hafla ya kutuza washindi akiwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na Gavana wa kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga kati ya wengine.
Timu hizo zimejishindia shilingi milioni 5 kila moja huku timu zinazofuata katika nafasi za pili, tatu na nne zikituzwa shilingi milioni 3, 2 na 1 mtawalia.