Saa chache tu baada ya kuondoa hoja ya mjadala wa kumbandua afisini Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza, mwakilishi wadi mteule Zippora Kinya amewasilisha hoja nyingine kwa nia sawa.
Hii ni mara ya tano hoja kama hiyo inawasilishwa katika bunge la kaunti ya Meru.
Wabunge wa bunge la kaunti ya Meru wamefanikiwa kumwondoa afisini Gavana Mwangaza mara mbili awali na akaokolewa na bunge la Seneti ambalo lilidai kwamba makosa aliyolimbikiziwa hayakutosha kumbandua afisini.
Wawakilishi wadi wanadai kwamba ilikuwa aibu kwao kwa mahakama kuu ya Meru kuamuru kwamba kesi yao itatuliwe na baraza la wazee wa jamii ya Ameru Njuri Ncheke.
Bunge hilo la kaunti ya Meru linasema kwamba suala linaloendelea ni la kikatiba na ilikuwa makosa kwa mahakama kuu mjini Meru kulichukulia kama suala la kiraia kwa kutaka mwingilio wa Njuri Ncheke.
Kulingana na hoja iliyowasilishwa leo, makosa anayolaumiwa kwayo Gavana Mwangaza ni yale yale yaliyokuwa kwenye hoja ya awali iliyotupiliwa mbali jana.
Yanajumuisha ukiukaji mkubwa wa katiba na sheria nyingine, ukiukaji mkubwa wa maadili na matumizi mabaya ya mamlaka.